Baadhi ya Waandishi waliohudhuria katika Mkutano wa Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Pindi Chana katika ukumbi wa Idara ya Habari leo Mjini Dodoma. |
(PICHA NA
HASSAN SILAYO)
Na Jovina
Bujulu, Maelezo Dodoma.
Wanafunzi nchini wametakiwa kuripoti katika sehemu husika
ikiwamo kwenye madawati ya kijinsia iwapo watakumbana na aina yeyote ya
udhalilishaji wa kijinsia.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Pindi Chana wakati wa Mkutano na waandishi wa
habari leo Mjini Dodoma.
Dkt. Pindi alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko kwa
wanafunzi hasa wa vyuo vikuu kukumbana
na udhalilishaji wa kijinsia katika kipindi cha utoaji wa matokeo ya mitihani.
“Tumekuwa tukipata malalamiko sana kwa wanafunzi wa hasa wa vyuo vikuu kukumbana na
udhalilishaji wa kijinsia hasa katika kipindi cha matokeo ila wito wetu kwao ni
kuripoti katika sehemu husika na Madawati ya kijinsia na sisi kama serikali
tunaahidi kusaidiana nao kutokomeza tatizo hili”Alisema Dkt. Pindi.
Akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa
Machi 8 kila mwaka Dkt. Pindi alisema kuwa dhumuni kuu la siku hii ni
kuiwezesha jamii kupima utekelezaji wa maazimia, Matamko, mikataba na itifaki
mbalimbali za kimataifa zinazohusu masuala ya wanawake ili kuhakikisha haki za
wanawake zinalindwa.
Aidha, Dkt. Pindi aliongeza kuwa wananchi hawana budi
kuongeza juhudi katika kufichua, kubaini na kuchukua hatua za kukomesha ukatili
na kunyimwa haki kwa wanawake kwani wanaofanyiwa hivi ni dada zetu, watoto
wetu, mama zetu na wengine ni bibi zetu.
Maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika ngazi za mikoa
kwa kila mkoa kuandaa utaratibu wa maadhimisho haya na kauli mbiu ya mwaka huu
ni “Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia”
No comments:
Post a Comment