Vibrant

Tuesday, 29 April 2014

UTUMISHI YATWAA UBINGWA MASHINDANO YA MEI MOSI 2014

Wachezaji wa Ofisi ya Rais, Utumishi wakipasha misuli moto (warm-up) jana kabla ya mechi ya mashindano ya Mei Mosi 2014 dhidi ya Uchukuzi iliyochezwa uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
Mfungaji bora wa mshindano ya Mei Mosi 2014 wa mpira wa pete Fatuma Machenga (GS) wa Utumishi akiwa na kikombe cha ufungaji bora mara baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi wakati wa hafla fupi ya ufungaji wa mashindano hayo iliyofanyika jana Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Baadhi ya wachezaji wa Utumishi (jezi za kijani) wakishangilia ubingwa wa michuano ya Mei Mosi waliopata pamoja na baadhi ya wanamichezo wenzao toka taasisi mbali mbali mara baada mechi dhidi ya Uchukuzi iliyochezwa jana uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.


Mchezaji wa Uchukuzi (C) (mwenye mpira) akijianda kutoa pasi kwa huku  mchezaji wa Utumishi Sophia Komba akijianda kuunyaka mpira katika mechi ya mashindano ya Mei Mosi 2014 dhidi ya Uchukuzi iliyochezwa jana uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.


Na. James Katubuka
Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeibuka kinara wa mpira wa pete katika mashindano ya Mei Mosi ya mwaka huu yaliyofikia tamati jana katika kiwanja cha Jamhuri mjini Morogoro.

Utumishi walijikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuisambaratisha timu ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuibugiza magoli 33 dhidi ya 21 katika mchezo uliokuwa na ushindani na msisimko wa aina yake uliorindima katika Uwanja mkongwe wa Jamhuri Morogoro.

Mchezaji Fatuma Machenga (GS) wa Ofisi ya Rais (Utumishi) alikuwa mwiba dhidi ya timu ya Uchukuzi kwa kuiongoza Utumishi vema katika mchezo huo.
Aidha,Goal Shooter (GS) huyo wa Utumishi ndiye mfungaji bora wa mashindano ya Mei Mosi kwa mpira wa pete ambapo amefunga magoli 136 yaliyopelekea kunyakua kikombe cha ufungaji bora.

Akizungumzia hali ya mchezo baada ya mwamuzi kupuliza kipenga cha mwisho, Mchezaji Subira Jumanne (WA) wa timu ya Uchukuzi alisema kuwa mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa kwani walikutana na timu nzuri na iliyojiandaa vema.
“Asiyekubali kushindwa si mshindani hivyo tutafanya maandalizi ya kutosha ili katika mashindano yajayo nasi tuwe mabingwa” alisema Subira.

Naye,mfungaji bora wa mshindano hayo mchezaji Fatuma Machenga (GS) wa Utumishi akiwa mwenye furaha alisema kuwa anajisikia fahari kuiwezesha timu yake kuwa bingwa.

“Tutahakikisha kuwa mwakani tunapambana kwa hali na mali ili tuweze kutetea ubingwa wetu” alisema Machenga.

Utumishi imenyakua kombe hilo lililokuwa likishikiliwa na timu ya Wizara ya Ulinzi ambao ndio walikuwa mabingwa wa Mei Mosi 2013.Kikombe cha mshindi wa pili  kwa mwaka huu kimenyakuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na mshindi wa tatu ni Wizara ya Uchukuzi.