Katibu Mkuu Utumishi Bw.George D. Yambesi (kushoto) akikabidhi ofisi kwa Naibu Katibu Mkuu Utumishi Bw.HAB Mkwizu baada ya kustaafu Utumishi wa Umma.Makabidhiano hayo yamefanyika ofisini kwake leo. |
Thursday, 26 March 2015
KATIBU MKUU UTUMISHI ASTAAFU UTUMISHI WA UMMA
Wednesday, 18 March 2015
MH.DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE AZINDUA KITUO CHA TAIFA CHA KUMBUKUMBU DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Muuungano
wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa Uzinduzi wa
Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma leo.
|
Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, viongozi wa Serikali na Washirika wa Maendeleo kwa pamoja wakikata utepe kuzindua Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma leo. |
Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiangalia moja ya faili lenye kumbukumbu za zamani katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma leo. |
HOTUBA
YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KATIKA
SHEREHE YA UFUNGUZI RASMI WA KITUO
CHA TAIFA CHA KUMBUKUMBU
DODOMA
TAREHE 18 MACHI, 2015
·
Waheshimiwa
Mawaziri,
·
Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
·
Waheshimiwa
Wabunge,
·
Waheshimiwa
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
·
Ndugu
Makatibu Wakuu,
·
Mheshimiwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Kumbukumbu
na Nyaraka za Taifa,
·
Mheshimiwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya
Mfuko wa Kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu,
·
Ndugu Viongozi wa Taasisi Mbalimbali za Serikali,
·
Ndugu Wanahabari,
·
Wageni Waalikwa,
·
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa kupata nafasi ya kualikwa ili kuja kushirikiana nanyi
katika tukio hili muhimu la ufunguzi rasmi wa Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu (The National Record Centre) hapa Dodoma.
Kipekee napenda kuipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa
kuandaa shughuli hii. Pia ninawashukuru wageni wote kwa kuja kushiriki katika tukio
hili muhimu.
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana, Ninaamini mtakubaliana nami kwamba, kumbukumbu ni
nyenzo muhimu katika utendaji kazi Serikalini na Taasisi zake. Bila ya kuwa na
kumbukumbu sahihi hatuwezi kujua tunakotoka na tunakokwenda na hivyo kushindwa
kufikia maamuzi sahihi kwa wakati. Kumbukumbu hutumika kama kielelezo katika
uwajibikaji na ni nguzo muhimu katika Utawala Bora. Ili Serikali iweze kufikia
lengo hilo na kuwezesha umma kujua mwenendo wa Serikali yao, lazima kuwe na kumbukumbu
zinazotunzwa vizuri na zinazopatikana kwa urahisi. Kukosekana kwa taarifa
sahihi na kwa wakati unaofaa kunaweza kuwafanya Watendaji wa Serikali kushindwa
kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa maamuzi
au kutolewa kwa maamuzi yasiyo sahihi na yasiyokidhi matarajio ya wananchi. Aidha,
ukosefu wa kumbukumbu hutoa mianya ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma,
matumizi mabaya ya madaraka na hata kuchelewesha au kuzuia haki kutendeka. Kasoro
hizi huchangia sana katika kuzorotesha maendeleo ya uchumi wa Taifa na
malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu Serikali yao na Taasisi zake.
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana, Programu
ya Mabadiliko katika Utumishi wa Umma awamu ya pili (Public Service Reform
Programme II – PSRP II) niliyoizindua mwezi Januari 2008, pamoja na mambo
mengine ilijielekeza katika kufanya
mabadiliko kwenye mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na utoaji wa taarifa katika
Utumishi wa Umma. Lengo kubwa la mabadiliko haya likiwa ni kuwa na Serikali
yenye kuwajibika, uwazi na utawala bora. Chini ya Programu hii, Serikali iliona
umuhimu wa kuangalia upya jinsi inavyozalisha taarifa zake, kuzitumia,
kuzitunza na kuzihifadhi kwa ajili ya matumizi ya sasa na ya baadaye. Aidha,
kabla ya uzinduzi wa Programu hii, Serikali ilibaini kuwepo kwa tatizo kubwa la
utunzaji wa kumbukumbu hasa mlundikano mkubwa wa majalada katika Ofisi za Umma,
ambayo yalihifadhiwa bila ya kufuata taratibu za utunzaji kumbukumbu. Hali hii kwa
kiasi kikubwa pamoja na mambo mengine iliathiri utendaji wa Serikali katika
kuwahudumia wananchi kama vile
ucheleweshaji wa kulipwa pensheni kwa watumishi wa umma, ugawaji holela
wa viwanja na ucheleweshaji wa kusikilizwa kesi, rushwa na upotevu wa mali za
umma. Kumbukumbu zinazotunzwa vizuri ni sawa na uti wa mgongo wa Serikali
katika kufikia malengo yake kwa ukamilifu katika kutunga na kutekeleza Sera
sahihi, kuweka mipango madhubuti, kuongeza ufanisi, tija, uwazi na uwajibikaji.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM ya mwaka
2010, inasisitiza upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wananchi ambao ndiyo
mamlaka iliyoiweka Serikali ya Awamu ya Nne madarakani. Aidha, Sera ya Taifa ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ya Mwaka 2010
na Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Na. 3 ya Mwaka 2002 zinaelekeza
Serikali na Taasisi zake kuwa na majengo na vifaa vinayokidhi uhifadhi bora wa
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Kituo hiki ni moja ya vielelezo vya juhudi za Serikali
katika kuhifadhi na kutunza kumbukumbu na nyaraka za Taifa ambazo ni dira ya
kizazi kilichopo na kijacho kama sehemu ya urithi andishi na historia ya Taifa
letu. Kuwepo kwa Kituo hiki, kutaongeza ufanisi katika utendaji na utoaji
huduma bora kwa wananchi kwani kitakuwa ni chimbuko la taarifa mbalimbali
zitakazoisaidia Serikali katika uendeshaji wa kazi zake za kila siku.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Miundombinu ya Kituo hiki ni ya Kisasa na itakuwa na
uwezo wa kuhifadhi majalada zaidi 770,000. Kutokana na uwezo wa Kituo kuhifadhi
majalada hayo, Taasisi za Umma zitaokoa zaidi ya mita za mraba 77,700 za ofisi
zao ambazo zilikuwa zikitumika kuhifadhi majalada haya. Aidha, miundombinu hii imezingatia
uzalishaji wa taarifa za Serikali katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),
hivyo Kituo kimeunganishwa na mkongo wa Taifa ili kurahisisha mawasiliano
Serikalini ikiwemo upatikanaji wa taarifa na nakala za kumbukumbu zitakazokuwa
zinahitajika na watumiaji mbalimbali kwa haraka na uhakika zaidi kutoka katika
Kituo hiki.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Sera ya Taifa ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ya
mwaka 2010 na Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Namba 3 ya mwaka 2002,
zinaagiza Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kusimamia taratibu na mifumo ya
utunzaji kumbukumbu, usalama wa kumbukumbu na nyaraka na kuwajengea uwezo
watumishi wa masjala katika kutunza na kuwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa
raia wake. Napenda nichukue nafasi hii kuwakumbusha Watendaji Wakuu wa Ofisi
mbalimbali za umma kuhusu wajibu wao wa kutunza kumbukumbu zinazozalishwa
katika Ofisi zao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali
inayotolewa na mamlaka husika. Watendaji Wakuu wa Taasisi zote za Serikali wahakikishe
wanahamishia katika Kituo hiki kumbukumbu zote zilizofungwa ili Kituo hiki
kiweze kutunza kumbukumbu kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Kazi iliyofanyika ya kusanifu, kujenga na kuweka
vifaa vya kisasa vya kuhifadhia kumbukumbu ni nzuri na ya gharama kubwa. Nachukua
nafasi hii, kuwaelekeza wote mnaosimamia uendeshaji wa Kituo hiki kuhakikisha
kwamba kinatunzwa na kufanya kazi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Serikali kwa upande wake itaendelea kutenga
bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutunza na kukiendeleza Kituo hiki ambacho ni
cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Kabla sijamaliza hotuba yangu, naomba niwashukuru Washirika
wetu wa Maendeleo kwenye Programu ya Mabadiliko katika Utumishi
wa Umma, ambao kwa kushirikiana na Serikali yetu wamechangia katika kufanikisha
ujenzi na uwekaji wa vifaa vya kisasa katika Kituo hiki. Kwa kutambua umuhimu wa kumbukumbu na nyaraka
walikubali kuchangia ujenzi wa Kituo hiki muhimu kwa nchi yetu. Hivyo, kwa
namna ya pekee ninawashukuru sana Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza kupitia
DfID na Serikali ya Canada kupitia CIDA kwa kuwezesha ujenzi wa Kituo hiki.
Mwisho
ninapenda niwashukuru wote mliohudhuria sherehe hii ya ufunguzi wa Kituo cha
Taifa cha Kumbukumbu - Dodoma. Ni
matarajio yangu kuwa Kituo hiki kitakuwa chachu ya kuleta uwajibikaji, uwazi na
utawala bora kwa Taasisi zote za Serikali.
Asanteni kwa kunisikiliza!!
Friday, 13 March 2015
KATIBU MKUU UTUMISHI ATEULIWA KUWA KAMISHNA TUME YA UTUMISHI WA UMMA
Thursday, 5 March 2015
VACANCY ANNOUNCEMENT
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
PRESIDENT’S OFFICE
PUBLIC SERVICE MANAGEMENT
Applications are hereby
invited from qualified and experienced Tanzanians for the following Vacant post
advertised by the Commonwealth
Secretariat.
(i) Director, Political Division
(i) Duty Station: London, United
Kingdom
(ii) Deadline for Applications: 16th March, 2015
SUBMISSION OF
APPLICATIONS:
- For more information regarding Terms of Reference of the advertised post; qualifications, tenure of appointment, and remuneration please visit the Commonwealth Secretariat’s website, (www.thecommonwealth.org/jobs).
- Applications must be submitted online to the address provided in the above mentioned website
- NB: appropriately qualified Women are highly encouraged to apply for this post.
- A copy of the application should be sent to:-
Permanent
Secretary,
President’s
Office - Public Service Management,
Human
Resources Development Division,
8
Kivukoni Road,
P.O.
BOX 2483,
11404 DAR ES SALAAM.
Fax No: + 255-22-2125299 or +
255-22-2127806
Email:
permsec@utumishi.go.tz
Subscribe to:
Posts (Atom)