Shirikisho la
Michezo Wizarani (SHIMIWI) limeandaa mafunzo ya uongozi,ualimu wa michezo na
huduma ya kwanza viwanjani kwa viongozi wa vilabu vya michezo ya SHIMIWI,yatakayofanyika
mjini Morogoro Februari 24-28 mwaka huu.
Hayo
yalisemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa SHIMIWI Bw.Moshi Makuka mapema leo ofisini
kwake alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa mikakati ya shirikisho hilo
kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Bw.Makuka
alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo kwa viongozi wa vilabu ni kuwajengea
uwezo wa kuongoza shughuli za michezo,kuwapa ufahamu zaidi juu ya katiba,sheria na kanuni za michezo ya SHIMIWI na
kuwapa uelewa wa namna ya kutoa huduma ya kwanza katika viwanja vya michezo.
Akielezea
sababu za Shirikisho hilo kuandaa mafunzo hayo Bw.Makuka alisema kuwa mafunzo hayo
yanafanyika kutokana na na changamoto zilizojitokeza katika mashindano ya
SHIMIWI ya miaka iliyopita ambapo baadhi
ya viongozi huvunja sheria na kanuni za michezo.
“Baadhi ya viongozi
wa SHIMIWI katika Wizara ,Idara Zinazojitegemea,wakala wa Serikali na Ofisi za
Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) wamekuwa wakilalamikiwa kutumia wachezaji ambao sio
watumishi wa umma .”alisema Bw.Makuka.
Pia,aliongeza
kuwa mafunzo hayo yatawahamasisha viongozi wa ofisi za Serikali zilizoshindwa
kushiriki katika michezo ya mwaka jana ili iweze kushiriki mwaka huu kwa kuwa
michezo kwa watumishi wa umma hujenga afya,mshikamano na pia huongeza ufanisi
mahala pa kazi.
Michezo ya
SHIMIWI ilianzishwa kwa madhumuni ya kuwakutanisha watumishi wa Serikali kwa
lengo la kujenga na kuendeleza
tabia ya ushirikiano,upendo na undugu hivyo hufanyika kila mwaka.Mafunzo
haya hufanyika kila mwaka kwa mujibu wa kalenda ya SHIMIWI.
No comments:
Post a Comment