Na Frank Mvungi-Maelezo
Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) imeanzisha utaratibu mpya wa kurejesha mikopo
kwa njia ya mtandao.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wabodi hiyo Cosmas
Mwaisobwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Mwaisobwa
amesema kuanzia mwezi Septemba, 2013 Bodi hiyo ilianzisha utaratibu mpya wa
kurejesha mikopo yao kupitia huduma ya M-Pesa.
Mwaisobwa alisema
katika kuimarisha mfumo wa urejeshaji mikopo kuanzia mwezi april, 2014
walionufaika na mikopo hiyo wataweza kurejesha kupitia Aitel Money.
Kabla ya kuanza kutumia
huduma ya M-pesa, mnufaika wa mkopo anapaswa kuwasiliana na HELSB ili kupata
mambo muhimu ambayo ni Taarifa ya Mkopo, (Loan statement) Kiwango cha
marejesho, (Loan instalments) na Namba ya kumbukumbu (Loan number).
HELSB pia hutoa msaada
kwa waombaji wa mikopo wanaopata matatizo madogo madogo wakati wa kujaza fomu
kwa kutumia dawati maalum la msaada kwa wateja ambapo msaada hutolewa kwa njia
ya simu siku za Jumatatu hadi Jjumaa kuanzia saambili asubuhi hadi saa 2 usiku.
Mwaisobwa alibainisha
baadhi ya changamoto zinazoikabili HELSB ni imani potofu iliyoenea kwamba
mikopo hiyo ni ruzuku na ushirikiano hafifu na baadhi ya waajiri katika
urejeshaji mikopo.
Mwaisobwa alitoa wito
kwa wale wote walionufaika na mikopo kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa
fursa kwa wahitaji wengine kukopeshwa.
Tangu kuasisiwa kwake, Bodi
hiyo imefanikiwa kutoa mikopo kwa idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na
hali ilivyokuwa kabla bodi kuanzishwa, ambapo wanafunzi wameongezeka kutoka
wanafunzi 42,729 mwaka 2005/2006 hadi wanafunzi 97,348 mwaka 2012/2013,ongezeko
hili ni sawa na wastani wa 10.4% kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment