Vibrant

Thursday 3 April 2014

TFDA YATOA MATOKEO YA UKAGUZI MAALUM WA MADUKA YA BIDHAA ZA VYAKULA JIJINI DAR, YAWATAKA WANANCHI KUJENGA UTARATIBU WA KUSOMA MAELEZO YA BIDHAA KABLA YA KUNUNUA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Bw.Hiiti Sillo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu ukaguzi maalum wa maduka ya kuuzia vyakula   “Supermarkets”
 na Mini-Supermarkets  katika jiji la Dar es salaam.

 Mkurugenzi wa Usalama na Chakula wa TFDA Bw. Raymond  Wigenge akitoa ufafanuzi kwa waandishi kuhusu hatua zinazochukuliwa na TFDA kuhakikisha usalama wa vyakula na Dawa nchini .TFDA imekuwa ikiongeza nguvu katika kukabiliana na bidhaa zisizokidhi viwango kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za udhibiti kwa kukagua, kukamata na kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha wanaokiuka sheria.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Bw.Hiiti Sillo (kulia) akitoa ufafanuzi wa baadhi ya bidhaa zilizokamatwa katika ukaguzi maalum kwenye maduka ya kuuzia vyakula   “Supermarkets” na Mini-Supermarkets  katika jiji la Dar es salaam zikiuzwa kinyume cha sheria ya Chakula , Dawa na Vipodozi sura ya 219. Wengine ni Mkurugenzi wa Usalama naChakula wa TFDA Bw. Raymond  Wigenge,na Meneja wa Ukaguzi wa Chakula wa TFDA kanda ya Mashariki Bw. Emmanuel Alphonce.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Bw.Hiiti Sillo (kulia) akitoa ufafanuzi wa maziwa yaliyokamatwa yakiwa kwenye kifungashio kisichokua na maelezo yoyote yakiuzwa kwenye maduka ya kuuzia vyakula   “Supermarkets”na Mini-Supermarkets  katika jiji laDar es salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Bw.Hiiti Sillo (kulia) akitoa ufafanuzi wa baadhi ya bidhaa zilizokamatwa katika ukaguzi maalum kwenye maduka ya kuuzia vyakula   “Supermarkets” na Mini-Supermarkets  katika  jiji la Dar es salaam zikiuzwa kinyume cha sheria ya Chakula , Dawa na Vipodozi sura ya 219. Wengine ni Mkurugenzi wa Usalama na Chakula wa TFDA Bw.Raymond  Wigenge, na Meneja wa Ukaguzi wa Chakula wa TFDA kanda ya Mashariki Bw. Emmanuel Alphonce.

 Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)Bi. Gaudensia Simwanza akiwaonesha waandishi wa habari baadhi ya bidhaa zilizokamatwa na mamlaka hiyo  zikiwemo chumvi, vinywaji, maziwa ya watoto ambazo hazijasajiliwa na mamlaka hiyo kufuatia ukaguzi maalum uliofanyika katika jiji la Dar es salaam.

 Maziwaya watoto aina ya SMA 1,2 na 3, Promil Gold, S-26 Gold, Nursoy, Progress Gold, Cow &Gate, Isomil 2 na Infacare Soya , Nutrikids na Aptimil 1 yaliyokamatwa ambayo hayajasajiliwa na TFDA .


 Vinywaji baridi ambavyo havikusajiliwa na TFDA vilivyokamatwa kufuatia ukaguzi maalum katika jiji la Dar es salaam.Picha na 10.Bidhaa za chumvi ambazo hazikusajiliwa na TFDA zilizokamatwakufuatia ukaguzi maalum katika jiji la Dar es salaam. 

 Na Gaudensia Simwanza ( TFDA)

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imetoa wito kwa  wananchi kujenga utaratibu wa kusoma maelezo ya bidhaa za vyakula zinazouzwa katika maduka mbalimbali nchini ili kubaini nchi zilikotengenezwa bidhaa husika,  muda wa matumizi na taarifa za uthibitisho wa bidhaa hizo kutoka mamlaka hiyo ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa zisizokidhi viwango.



 Hatua hiyo imekuja kufuatia ukaguzi wa maduka 107 ya bidhaa za vyakula (supermarkets),uhakiki wa uwepo wa vibali vya biashara na ukamataji wa bidhaa za chakula ambazo hazijasajiliwa na kupewa idhini ya kutumika hapa nchini uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa kuanzia tarehe 10 Marchi hadi 21 mwaka huu katika jiji la Dar es salaam.


 Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Bw.Hiiti Sillo amesema kuwa vyakula mbalimbali vimebainika kuingizwa nchini, kusambazwa na kuuzwa katika maduka ya vyakula “Supermarkets” na Mini-Supermarkets zilizopo katika jiji la Dar es salaam kinyume cha sheria ya Chakula , Dawa na Vipodozi sura ya 219.

 Amesema kuwa TFDA imebaini na kukamata bidhaa mbalimbali za vyakula ikiwa ni sehemu ya utekezwaji wa sheria ya Chakula , Dawa na Vipodozi Sura ya 219 pia utekelezaji wa jukumu la kudhibiti usalama, ubora na ufanisi wa chakula, Dawa, Vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya ya jamii kwa kuzuia athari ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.

 Ameeleza kuwa katika ukaguzi huo jumla ya maduka 36 yalikutwa yakiuza maziwa ya watoto aina ya SMA 1,2 na 3, Promil Gold, S-26 Gold, Nursoy, Progress Gold, Cow &Gate, Isomil 2 na Infacare Soya , Nutrikids na Aptimil 1 ambayo hayajasajiliwa na TFDA na pia kukosa maelezo ya lugha ya kiswahili .

 “Napenda kufafanua kuwa  maziwa haya yaliyokamatwa ikiwa ni pamoja S-26 Gold na Progress Gold pamoja na kutosajiliwa
hayana maelezo katika lugha ya Kiswahili na yana picha na
 michoro ambayo hairuhusiwi kwa mujibu wa kanuni ya maziwa ya watoto” Amesema Bw. Siilo.

 Amesema kuwa katika ukaguzi huo maduka 12 yamekutwa yakiuza vinywaji vya kuongeza nguvuambavyo havijasajiliwa na TFDA vikiwemo Monster, B52, Krazy, Relentless, Boost, Redbull (red, silver&blue editions),Rockstar ,Climax pamoja na kinywaji aina ya Atlas.

 Aidha ameeleza kuwa jumla maduka 39 jijini Dar es salaam yamekutwa yakiuza chumvi zinazokiuka kanuni za uwekaji wa madini Joto kwenye chumvi ya mwaka 2010 na ambazo hazijasajiliwa na mamlaka hiyo zikiwemo Lo Salt, American Garden Salt, Ken Salt, Saxa, Chilly Willy Salt na kutoa wito kwa wananchi kutumia chumvi zilizowekewa  madini joto ambayo ni muhimu kwa afya ya mwanadamu.

 “Nawaomba wananchi kote nchini kutumia chumvi zilizowekewa madini joto zenye maneno  “Iodated Salt”  zilizosajiliwa na TFDA na kukidhi kanuni ya Uwekaji Madini joto kwenye chumvi ,2010” Amesisitiza.

Bw. Sillo amefafanua kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imebaini jumla ya maduka 39 (Supermarkets) yaliyokuwa yakiendesha shughuli zake  bila kuwa na vibali vya biashara na kubaini uuzwaji  wa vinywaji baridi  vyenye ladha ya matunda vikiwa sokoni ambavyo vilikuwa na picha za matunda kuainisha kuwa vimetengenezwa kwa matunda halisi kinyume cha kanuni za vielelezo ya mwama 2006.

 “Katika ukaguzi wetu pia tumebaini uwepo wa bidha zenye taarifa ambazo sio sahihi hasa za vinywaji baridi zenye vifungashio vyenye picha za matunda kuashiria kuwa vimetengenezwa kwa matunda halisi na pia soda za kopo ambazo hazikuandikwa kwa lugha ya Kiswahili wala kiingereza hii ni kinyume cha utaratibu hatuwezi kuruhusu hali hii na TFDA tutaendelea kufanya ukaguzi ili kulitokomeza tatizo hili”
 Ameeleza kuwa kufuatia hali hiyo Mamlaka imechukua  hatua mbalimbali ikiwemo kukamata na kuharibu makopo 591 ya maziwa ya watoto yenye thamani ya shilingi milioni 17.5, ukamataji wa makopo1526 ya vinywaji vya kuongeza nguvu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 4 nakukamatwa kwa pakiti 6090 za chumvi zenye ujazo tofauti zenye thamani ya shilingi milioni 5 ambazo zinasubiri kuharibiwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha Katika kukabiliana na tatizo la kuibuka kwa wimbi la uingizaji wa bidhaa hasa maziwa ya watoto na ufunguaji wa maduka (supermarkets na Mini-Supermarkets) kinyume cha sheria amesema TFDA inaendelea kushirikiana na taasisi zinazofanya kazi ya udhibiti zikiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kukabiliana na vitendo vya baadhi ya watu wanaokiuka sheria kwa kuingiza bidhaa zisizokidhi viwango na ambazo hazijasajiliwa kupitia maeneo yasiyo rasmi mipakani (njia za panya).

 Amesema wanaokamatwa kwa makosa ya kuuza bidhaa zisizosajiliwa na mamlaka wanachukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo  kuteketeza bidhaa zao , kufunga biashara zao na kuwafikisha mahakamani kwa kukiuka sheria na kanuni za Mamlaka ya Dawa na Chakula.
Amewataka wananchi wanaotaka kufungua maduka makubwa ya kuuzia bidhaa za vyakula, dawa,vipodozi na vifaa tiba kuwasiliana na Mamlaka ya Chakula na Dawa ili waweze kupata vibali vya kuwawezesha kufanya kazizao kwa kufuata sheria na kanuni.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama na Chakula wa TFDA Bw.  Raymond  Wigenge ameeleza kuwa katika kuhakikisha usalama wa vyakula na Dawa nchini TFDA imekuwa ikiongeza nguvu katika kukabiliana na bidhaa zisizokidhi viwango kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za udhibiti kwa kukagua, kukamata na kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani wanaokiuka sheria.

“Sisi tunafanya kazi zetu kwa mujibu wa sheria,mpaka sasa tuna kesi zaidi ya 200 za makosa ya kukiuka sheria na kanuni za Mamlaka ya Chakula na Dawa”

Naye Meneja wa ukaguzi wa usalama wa chakula wa Mamlaka wa Chakula na Dawa Nchini Bw. Justin Makisi ameeleza kuwa kufuatia kuendelea kwa zoezi la kukagua maduka katika maeneo mbalimbali na adhabu zinazotolewa na mamlaka kwa mujibu wa sheria kwa wale wanaovunja sheria baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa kuchukua hatua  za kutimiza masharti yote wanayopewa na TFDA.

 “ Tunapowachukulia hatua wale wanaokutwa na makosa mbalimbali hasa kuyafunga maeneo ya biashara zao kwa kukiuka masharti baadhi yao hutimiza kanuni na sheria zilizowekwa wengi na kuruhusiwa kuendelea na biashara zao.


No comments: