Wachezaji wa Ofisi ya Rais, Utumishi wakipasha misuli moto (warm-up) jana kabla ya mechi ya mashindano ya Mei Mosi 2014 dhidi ya Uchukuzi iliyochezwa uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro |
Na.
James Katubuka
Ofisi ya Rais,Menejimenti ya
Utumishi wa Umma imeibuka kinara wa mpira wa pete katika mashindano ya Mei Mosi
ya mwaka huu yaliyofikia tamati jana katika kiwanja cha Jamhuri mjini Morogoro.
Utumishi walijikita kileleni
mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuisambaratisha timu ya Wizara ya Uchukuzi
kwa kuibugiza magoli 33 dhidi ya 21 katika mchezo uliokuwa na ushindani na
msisimko wa aina yake uliorindima katika Uwanja mkongwe wa Jamhuri Morogoro.
Mchezaji Fatuma Machenga
(GS) wa Ofisi ya Rais (Utumishi) alikuwa mwiba dhidi ya timu ya Uchukuzi kwa
kuiongoza Utumishi vema katika mchezo huo.
Aidha,Goal Shooter (GS) huyo
wa Utumishi ndiye mfungaji bora wa mashindano ya Mei Mosi kwa mpira wa pete
ambapo amefunga magoli 136 yaliyopelekea kunyakua kikombe cha ufungaji bora.
Akizungumzia hali ya mchezo
baada ya mwamuzi kupuliza kipenga cha mwisho, Mchezaji Subira Jumanne (WA) wa timu
ya Uchukuzi alisema kuwa mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa kwani walikutana na
timu nzuri na iliyojiandaa vema.
“Asiyekubali kushindwa si
mshindani hivyo tutafanya maandalizi ya kutosha ili katika mashindano yajayo nasi
tuwe mabingwa” alisema Subira.
Naye,mfungaji bora wa
mshindano hayo mchezaji Fatuma Machenga (GS) wa Utumishi akiwa mwenye furaha
alisema kuwa anajisikia fahari kuiwezesha timu yake kuwa bingwa.
“Tutahakikisha kuwa mwakani
tunapambana kwa hali na mali ili tuweze kutetea ubingwa wetu” alisema Machenga.
Utumishi imenyakua kombe
hilo lililokuwa likishikiliwa na timu ya Wizara ya Ulinzi ambao ndio walikuwa
mabingwa wa Mei Mosi 2013.Kikombe cha mshindi wa pili kwa mwaka huu kimenyakuliwa na Wizara ya
Mambo ya Ndani na mshindi wa tatu ni Wizara ya Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment