Vibrant

Wednesday 26 March 2014

TAMKO RASMI LA MTANDAO WA WATU WA PEMBA WAISHIO TANZANIA BARA

NEPPELTA
NETWORK FOR PEOPLE OF PEMBA LIVING IN TANZANIA MAINLAND
MTANDAO WA WATU WA PEMBA WAISHIO TANZANIA BARA

MAKUNGANYA STREET/ KARIAKOO
P.O. BOX 21243
DAR ES SALAAM
23/03/2014


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
TAMKO RASMI LA KUUNGA MKONO HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MH. DK. JAKAYA MRISHO KIKWETE LIYOITOA KWA BUNGE MAALUMU LA KATIBA, DODOMA TAREHE 21/03/2014.

Ndugu,
          Waandishi wa habari, Tunamtanguliza Mwenyezi Mungu mwingi wa rehemu, heri na Baraka.
Mpango wa kuunganisha nchi za Zanzibar na Tanganyika ambao mchakato wake ulianza mwaka 1963 ulikuwa ni utashi wa Viongozi wetu wawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Aman Karume.
Wote wawili kupitia vikao vyao mbalimbali walikubaliana kuziunganisha nchi hizi kwa maslahi mema ya wananchi wao. Hatua hiyo ilipewa Baraka na Mabunge ya nchi hizi mbili na miswada ya sheria ya kuunganishwa ilipitishwa na ikatungwa sheria iliyopelekea kufanyika tendo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 24 Aprili 1964.
Dhima ya Muungano wetu pamoja na mambo mengine ni kuimarisha historia ya vizazi vya nchi hizi mbili ambazo zina asili zinazofanana na historia za asili hizi zilivurugwa na Wakoloni wa Kijerumani, Kiingereza na hatimaye utawala wa Sultan.
Tangu Muungano ufanyike kumekuwa na mabadiliko mbalimbali hasa katika mahusiani ya kibiashara.
Sisi Watanzania wenye asili ya Pemba tunaoishi huku Bara tumefaidika na tunaendelea kufaidika sana na uwepo wa Muungano. Ukiachilia suala la ajira za Serikalini, Muungano umesaidia kukua kwa biashara zetu ambapo mtaji wa Wapemba pekee wanaoishi huku umeweza kufikia shilingi Trilioni 1.2. Hiki si kiasi kidogo kwa nchi kama Tanzania inayopigania ukuaji wa uchumi kupitia mitaji ya uwekezaji hasa wa kizalendo.
Idadi ya Wapemba wanaoishi Bara imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo hadi mwaka 2012 inakadiriwa kwa kufikia laki 8.3. Faida nyingine pia ni sisi kuoa au kuolewa na wenzetu wa Bara hali iliyochangia kuongezeka kwa mahusiano ya kindugu. Pia Wapemba wamejihusisha zaidi na Kilimo na ufugaji na kuongeza tija zaidi katika sekta hizo.
Hivyo basi kuwepo kwa dalili zozote za kuvunjika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hakuwezi kutuacha salama sisi Wapemba tuishio huku Bara. Chokochoko zote na ishara mbaya za chuki kati ya Wabara na Wazanzibar hazitaweza kuimalisha msingi mkubwa wa Muungano uliojengwa kwa muda mrefu chimbuko lake likiwa ni waasisi wetu.
Kwa hatua hiyo basi mtandao wetu umeona si vyema kukaa kimya bila kumpongeza Rais wetu Dk. Jakaya Kikwete kwa hotuba nzuri iliyojaa hekima, busara, uzalendo na upole. Sisi tumefarijika sana Rais wetu kukemea Serikali tatu kwa kuonyesha udhaifu wa kila mmoja huku akijenga hoja zenye mshiko kuhusu athari za Serikali hizo kwa uwepo wa Muungano huu.
Tumeamini kweli kupitia hotuba yake Mh. Dk. Kikwete ana nia ya dhati ya kulinda Muungano kama alivyoapa tangu amakabidhiwa nchi hii.
Sisi Wapemba tuishio Bara tunamhakikishia Rais wetu kuwa tutapambana na hila zozote za wenye nia mbaya ya kutaka kuvunja Muungano aidha kwa itikadi za kisiasa, kidini, kikabila au uchu wa kutawala.



No comments: